21 Novemba 2013 - 20:30
Kusafisha uranium ni msimamo usiojadiliwa kwenye mazungumzo ya nyuklia

Mwakilishi wa Iran kwenye mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea mjini Geneva, Bw. Abbas Araqchi amesema, kusafisha uranium ni kanuni ambayo haitajadiliwa kwenye mazungumzo hayo.

Ripoti ya ABNA- Akizungumza na waandishi wa habari nchini humo, Araqchi amesema, ingawa suala la kusafisha uranium halitajadiliwa, lakini mambo mengine yote kuhusiana na uranium ikiwemo kiwango, mahali, na kiasi cha uranium inayosafishwa vinaweza kujadiliwa. Amesema nchi hiyo haitaingia kwenye makubaliano yoyote mpaka pale usafishaji wa uranium nchini Iran utazungumzwa kuanzia hatua zake za mwanzo mpaka mwisho.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, jana alisema, uamuzi wowote utakaofanywa au usipofanywa na nchi yoyote wa kusafisha uranium, au kama inaruhusiwa kufanya hivyo au la, na kama inaruhusiwa chini ya kanuni, vyote hivyo vinategemea majadiliano.